UNIVERSITY OF DAR ES SALAAM
CONFUCIUS INSTITUTE (CI)

News

Recently,Professor Aldin Mutembei, Dean of CI UDSM, published an article in the local mainstream media.The following is the article he published.

 

Urafiki baina ya Tanzania na China Unavyoendelezwa

 

Urafiki kati ya Tanzania na China, umedumu kwa zaidi  ya miaka 55 sasa. Huu ni urafiki uliojengwa kwa kuaminiana, kupendana na kushirikiana. Kwa Tanzania urafiki huu ulianza wakati wa chama cha TANU na umeendelezwa sasa ndani ya CCM, ambapo kwa China umeanzishwa na kuendelezwa na Chama cha Kikomunisti cha China. Ni urafiki unaojengwa katika siasa zinazolenga kuwaletea wananchi wote maendeleo bia ya kujali, rangi, jinsia au dini. Huu ni urafiki ulioanzishwa na Mwl. Julius Nyerere, Baba wa Taifa la Tanzania na Mwenyekiti Mao Tse Tung. Tokea wakati huo hadi leo umekuwa ni urafiki ambao umeheshimu utamaduni na lugha za mataifa haya mawili.

Kwa upande wa Tanzania, lugha ya Kiswahili iliyotangazwa rasmi kuwa lugha ya Taifa mwaka 1962, imekuwa kiungo cha umoja wa Watanzania na kielelezo cha utambulisho wa Watanzania. Leo hii, lugha ya Kiswahili imevuka mikapa ya kijiografia na kuenea Sehemu mbalimbali Afrika. Ilipokubalika kuwa mojawapo ya lugha rasmi za Umoja wa Afrika ilikuwa inajenga misingi ya kukubaliwa kuwa lugha yenye uwezo wa kuwasemea na kuwawakilisha Waafrika. Katika hili nchi ya China imeunga mkono kuenea kwake ncdani ya Taifa hili kubwa duniani.

Nchini China, lugha ya Kichina ya Mandarini, kama ilivyo Kiswahili kwa Tanzania, imewaunganisha Wachina wote na kuwapa sauti moja. Lugha hii ya Kichina inaenea kwa kasi duniani kote kupitia Taasisi zinazobeba jina la Confucius. Kwa sasa Taasisi hizi za Confucius ziko zaidi  ya 550 duniani kote na zinaendelea kuongezeka. Labda ni vema kujua huyu Confucius alikuwa nani.

Confucius, au kama aitwavyo na Wachina wenyewe, Kongzi alikuwa Mwalimu, Mwanafalsafa na Mwanasiasa aliyeamini katika kujenga nchi yenye maadili na yenye elimu bora. Alifundisha kuwa ili mtu uwe mwananchi bora katika nchi yako, huna budi kuwa mwenye kupenda elimu, mnyenyekevu, mtii na unayependa kufanya kazi. Aliishi katika karne ya 6 kabla ya kuzaliwa Yesu Kristo na anasadikiwa alifariki mwaka 479 KK akiwa na umri wa miaka 72. Alikuwa ni msingi mkubwa wa mawazo yanayotawala China hadi leo hii, na mtazamo wake wa maisha na uchapakazi wake umewaathiri Wachina hadi leo.

Kwa mtazamo wake kuhusu elimu, Taasisi zinazofundisha lugha na utamaduni wa Kichina zilianzishwa na kupewa jina lake mwaka 2004. Taasisi hizi hufundisha lugha na utamaduni wa Kichina kwa kushirikiana na Vyuo na Taasisi za Kielimu sehemu mbalimbali duniani.

Hapa Tanzania, ushirikiano wa namna hii upo Chuo Kikuu cha Dodoma ambapo uanzishwaji wake ni kwa kushirikiana na Taasisi ya Zhengzhou inayojishughulisha na viwanda vya mambo ya anga. Uhusiano huu ulianzishwa mwaka 2012.  Taasisi ya Confucius pia ipo Dar es Salaam ambapo Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kilishirikiana na Chuo Kikuu cha Ualimu cha Zhejiang Normal kuanzisha Taasisi ya Confucius mwaka 2013.

Kwakuwa urafiki wa Tanzania na China umejengwa katika misingi ya kushirikiana, lugha ya Kichina inafundishwa nchini Tanzania na wakati huo huo lugha ya Kiswahili inafundishwa nchini China. Kwa sasa hakuna Taasisi inayosimamia ufundishwaji wa Kiswahili nchini China kama ilivyo kwa Taasisi za Confucius zinazofundisha Kichina mahali mbalimbali duniani. Hata hivyo, lugha ya Kiswahili inafundishwa katika Vyuo vikuu vipatavyo sita sasa na inaendelea kuenea kwa kupendwa na Wanafunzi wengi Wachina, kama inavyofundishwa katika nchi kadha za Asia. Kiswahili kilianza kufundishwa mwaka 1960 katika Chuo cha Mawasiliano cha China - (CUC).  Baadaye mwaka 1961 Chuo Kikuu cha Masomo ya Kigeni cha Beijing - (BFSU) nacho kikaanza kufundisha Kiswahili. Kwa sasa vyuo vingine ni:

  1. Tianjin Foreign Studies University - TFSU
  2. Luoyang Foreign Studies University tangu 2008
  3. Shanghai International Studies University (SISU) tangu 2018 ambacho sasa kimeanzisha Programu ya digrii ya awali ya Kiswahili (BA in Kiswahili),
  4. Xi’an International Foreign Studies University, tangu 2020.

 

Kwakuwa sasa Kiswahili kinazidi kuenea mahali pengi, haitashangaza kuona Vyuo vingi nchini China vikianzisha masomo ya lugha ya Kiswahili. Kwa Wachina, kujua lugha ya Kiswahili ni kuwafungulia fursa si tu kwa hapa Tanzania, bali na kwa Afrika nzima, maana lugha ya Kiswahili inaenea Afrika. Lakini kupitia lugha ya Kiswahili, lililomuhimu zaidi  kwa Wachina ni fursa ya kuwafahamu Waafrika.

Kupitia lugha ya Kiswahili, Wachina wanaendelea kujifunza mila na tamaduni za Kiafrika (hasa Wabantu). Mila na Desturi nyingi za Wabantu, ambao sasa ni zaidi  ya watu milioni 310, zinafanana. Kupitia lugha ya Kiswahili mila hizi zinafahamika nje ya mataifa yasiyo ya Kibantu. Ni kama ilivyo lugha ya Kichina, kuwa wanaojifunza lugha hiyo wanapata fursa ya kuwaelewa Wachina.

Kupitia Taasisi ya Confucius, mila na tamaduni za Kichina zinaendelea kujulikana. Jambo hili ni muhimu sana kwa mustakabali wa uwiano wa kidunia. Zamani, kabla ya milango ya mageuzi ya kiuchumi kufunguliwa, nchi za Kiafrika zilizotawaliwa zilielekezwa na kufahamu zaidi  tamaduni za nchi za Kimagharibi hasa Ufaransa, Uingereza, Ureno, Uhispaniola, Ujerumani na Marekani kuliko tamaduni za nchi nyingine zozote. Lakini tangu wakati wa biashara huria na kutanuka kwa utandawazi, nchi za Kiafrika zimepata fursa ya kuujua ustaarabu na uungwana wa nchi za Asia na hasa China. Kabla yake, ukitoa nchi ya Tanzania ambayo urafiki baina yake na China ulianza zaidi  ya miaka 55 iliyopita, kwa nchi nyingi, China ilikuwa ikijulikana kwa mbali kupitia vitabu vilivyoandikwa na wataalamu wa nchi za magharibi. Waafrika tulisoma na kuelezwa kuhusu China ya Kijamaa na Kikomunisti, nchi ya watu fukara na isiyoendelea. Lakini sasa kupitia Confucius, ulimwengu unaifahamu China kupitia kwa Wachina wenyewe. Ulimwengu unaifahamu China iliyopiga hatua kubwa kiuchumi, kiteknolojia, kielimu na hata kijamii. Kwa hakika kupitia Taassisi za Confucius duniani, ulimwengu unautambua uzuri wa Ukomunisti wa Kichina, na kutambua changamoto za maendeleo na namna wananchi wanavyohimizwa kujitatulia matatizo yao wenyewe. Tunafahamu kuwa China ni taifa kubwa duniani, lenye nguvu za kiuchumi na kiteknolojia duniani. Mambo haya hayakujulikana hapo kabla. Ni kupitia pia katika mitandao na Vyombo vya habari ambapo ulimwengu umeendelea kuifahamu China kwa undani.

Moja ya Vyombo vya habari kuhusiana na lugha ya Kiswahili ni Radio ya Kimataifa ya China – CRI. Radio hii iliyoanza kurusha matangazo ya Kiswahili mwaka 1961, inashirikiana na Taasisi za Confucius katika kuwaletea wasikilizaji habari kwa Kiswahili Mkondoni. Radio hii hurusha vipindi vya Kiswahili kwa saa 17 kila siku na hivyo kuifanya iwe miongoni mwa Radio kubwa duniani zinazorusha matangazo kwa Kiswahili.

Ujio wa Waziri wa Mambo ya Nje wa China, na desturi inayojengeka sasa kwa miaka mitatu mfululizo ya kuanza mwaka kwa kuitembelea Afrika, inaendeleza na kudumisha urafiki huu unaoendelea kuimarika baina ya Tanzania na China na hivyo kufungua fursa za kiutalii na kibiashara, kielimu na kijamii baina ya Tanzania na China.

Taasisi ya Confucius ya Chuo Kikuu cha Dar es salaam, imeanzisha mkakati wa kuandika na kuchapisha vitabu na makala ili kuvutia utalii wa China kwa Tanzania na kuendeleza lugha ya Kiswahili kwa Wachina. Taasisi pia inatafsiri vitabu kuhusu kilimo na mbinu za ukulima wa kisasa kutoka katika lugha ya Kichina kuingia katika lugha ya Kiswahili ili kuwawezesha wakulima wa Tanzania kufahamu mbinu za ukulima wa mazao mbalimbali na kupata faida ya kilimo chao. Tunakoelekea, kuna mwanga wa maisha bora kwa upande wa lugha ya Kiswahili na lugha ya Kichina duniani.

 

Prof. Aldin Mutembei. Mkurugenzi Mtanzania Taasisi ya Confucius