Uvaaji wa mavazi yanayozingatia maadili siyo jambo geni kwa watumishi wa umma na jamii kwa ujumla. Mwongozo wa uvaaji wa kuzingatia maadili kwa watumishi wa Umma ulitolewa na Serikali kwa mara ya kwanza kupitia Waraka Na. 1 wa mwaka 1971. Madhumuni ya Waraka huo ilikuwa ni kuimarisha heshima ya Taifa kwa kuhakikisha kuwa watumishi wa Serikali wanavaa mavazi ya heshima wanapowahudumia wananchi. Waraka huo uliainisha baadhi ya mifano ya mavazi ambayo yalionekana hayafai na yale yanayofaa kwa wanawake na wanaume, utengenezaji wa nywele unaofaa na usiofaa na vipodozi visivyokubalika.